by Elisha K. Mdumi
Niliposikia Sauti: Maisha Yangu Katika Huduma ya Mungu ni tawasifu ya Mchungaji Mstaafu Elisha K. Mdumi, inayosimulia safari ya maisha yake tangu kuzaliwa na kukulia katika jamii ya Wazaramo, kuupokea Ukristo, kuitikia mwito wa kumtumikia Mungu, kupata mafunzo ya Biblia na kichungaji, hadi kuhudumu katika maeneo mbalimbali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT). Kwa mtazamo wa uzoefu wake binafsi, mwandishi anaeleza changamoto, mafanikio na mafunzo aliyoyapata katika huduma, ikiwemo kipindi chake cha utumishi wa kimisioni Zanzibar, pamoja na mchango wake katika ujenzi na maendeleo ya huduma za Kanisa. Tawasifu pia inagusa historia ya KKKT, kazi za kimisioni na umuhimu wa kutunza kumbukumbu za Kanisa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Zaidi ya kuwa simulizi ya maisha binafsi, chapisho hili linatoa tafakari ya kitheolojia kuhusu mwito, utume wa Kanisa (Missio Dei), umoja wa Kanisa, huduma kamilifu kwa mwanadamu—kiroho, kiakili na kimwili—pamoja na changamoto ya kujenga Kanisa lenye uwezo wa kujiendesha, kujiongeza na kujitegemea. Kupitia kumbukumbu, matukio na maono aliyoyakusanya katika miaka mingi ya utumishi, Mch. Mdumi anawaalika wasomaji kutafakari nafasi ya uaminifu kwa wito wa Mungu, ushirika wa Kanisa na wajibu wa kizazi cha sasa katika kuendeleza urithi wa kiroho na kihistoria wa Kanisa.